WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema uandikishaji upya wa Daftari la Wapigakura, utafanyika kwa muda uliopangwa, ikiwemo kura ya maoni ya Katiba mpya Inayopendekezwa.
Alisema ni kweli mchakato huo umekumbwa na matatizo ya kifedha na hadi sasa wako tayari kuweka fedha katika mradi huo na kufanya kazi kwa juhudi ili lengo hilo liweze kutimia.
Alisema ratiba waliyopewa na Tume ya Uchaguzi (NEC), kuhakikisha mchakato huo unafanyika bila mizengwe kama ilivyopangwa ndiyo inaongoza serikali.
Pinda alikuwa akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambaye ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (CHADEMA) aliyeuliza suala la uandikishaji mpya wa wapigakura umekuwa ukiahirishwa kwa zaidi ya mara nne na kuelezwa kuanza leo, lakini hakuna dalili.
Hata hivyo, NEC ilishaanza majaribio ya uandikishaji kwa kutumia mfumo mpya wa kielektroniki katika majimbo ya Mlele, Kilombero na Kawe. Hata hivyo, majaribio hayo yalionesha matatizo, huku NEC ikitangaza kuanza uandikishaji Februari 15, mwaka huu.
Hivyo aliuliza ikiwa imebakia miezi mitatu kwa kura za maoni na miezi minane ya uchaguzi mkuu ni kwa jinsi gani serikali ina mpango wa kutoa muda kwa ajili ya uandikishaji huo kwa ajili ya uchaguzi mkuu pekee ili usionekane kuwa na matatizo.
“Mimi naamini kuwa zoezi hili litakamilika kama tume ilivyopanga na kwamba ni lazima ushirikishwaji wa kutosha hasa vyama vya siasa hivyo tunachoomba ni Tume kukaa na viongozi wa vyama vya siasa katika kila hatua kuhakikishiwa mchakato unavyokwenda naamini tukifanya hivyo tutafanikiwa, ”alisema Waziri Mkuu akijibu swali hilo.

Facebook Blogger Plugin by AllyTz

Post a Comment

 
Top