Maandalizi hafifu ya watahiniwa wa mitihani kwa ngazi zote ndio chanzo kikubwa cha kuwapo udanganyifu katika mitihani ya mwisho.
Hayo
yamebainishwa na Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala wa Baraza la
Mitihani ya Tanzania (Necta), Daniel Mafie aliyekuwa akizungumzia
mafanikio ya baraza hilo kwa niaba ya Katibu Mtendaji.
Alisema
pamoja na kupungua kwa watahiniwa wanaofanya udanganyifu kwenye
mitihani, lakini maandalizi hafifu ya wanafunzi wanachangia tatizo hilo.
“Unakuta
mtahiniwa hajajiandaa vizuri na hapo hapo anataka kuwa na matokeo
mazuri, hilo ndilo linalowafanya kuingia katika udanganyifu. Jamii
inatakiwa kujua njia pekee ya kufanya vizuri katika mitihani ya mwisho
ni kuwa na maandalizi mazuri,” alisema.
Alisema,
Baraza lake kwa kushirikiana na Kamati za Uendeshaji wa Mitihani katika
ngazi za Mikoa na Wilaya na wasimamizi wameweza kudhibiti tatizo la
wizi wa mitihani kwa kiasi kikubwa.
Alitolea
mfano mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, udanganyifu umepungua kutoka
watahiniwa 9,736 wa mwaka 2011 hadi mtahiniwa mmoja mwaka 2014, wakati
Kidato cha Nne ni watahiniwa 3,303 kwa mwaka 2011 hadi watahiniwa 184
kwa mwaka 2014.
Katika
matokeo ya mwaka 2014 yaliyotangazwa hivi karibuni kati ya watahiniwa
184 ambao matokeo yao yalifutwa kwa udanyanyifu, watahiniwa 128 walikuwa
ni watahiniwa wa kujitegemea katika vituo viwili na watahiniwa 56
wakiwa ni watahiniwa wa shule.
Kwa upande wa Kidato cha Sita udanyanyifu umepungua kutoka watahiniwa 11 kwa mwaka 2011 hadi watahiniwa watatu mwaka 2014.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment