Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) ameshindwa kuwasilisha hoja binafsi, kuitaka Serikali iwasilishe bungeni ripoti ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kuhusu uchunguzi wa tuhuma za rushwa katika sakata la iliyokuwa Akaunti ya Tegeta Escrow.
Lengo
la hoja hiyo kwa mujibu wa madai ya Kafulila, ilikuwa kuwezesha Bunge,
kufanya uamuzi mwingine wa alichoita ni uchunguzi mpana na wa kina.
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na Bunge kwenda kwa mbunge huyo, jana, Bunge limezuia hatua hiyo ya Kafulila, kwa sababu ilikuwa inakiuka Kanuni za Bunge.
Utaratibu
uliowekwa na kanuni ya 54 (4) ya Kanuni za Bunge toleo la 2013,
umekataza hoja iliyokwishaamuliwa na Bunge, isijadiliwe ndani ya miezi
12 isipokuwa kama ni hoja ya kutaka uamuzi huo wa Bunge
uliokwishafanyika ubadilishwe.
Katika
barua hiyo iliyosainiwa na Pius Mboya, kwa niaba ya Katibu wa Bunge,
imeeleza kwa kuwa hoja ya Kafulila haikusudii kutaka uamuzi huo
ubadilishwe, haikubaliki kikanuni.
Barua
hiyo ilieleza kuwa suala hilo lilijadiliwa na kuhitimishwa na Bunge
katika mkutano wa 16 na 17 na kutolewa maazimio yanayotakiwa kutekelezwa
na serikali, ikiwa ni pamoja na Takukuru.
“Tunapenda
kukujulisha pia kwamba hakuna ibara yoyote ya Katiba wala kifungu
chochote cha Sheria, kinacholipa Bunge madaraka ya kuitaka Serikali
iwasilishe bungeni ripoti yoyote ya kiuchunguzi ya Takukuru, ili
ijadiliwe bungeni,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Awali
akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kafulila alisema ripoti
iliyojadiliwa awali ilikuwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
ambayo inaangalia upungufu wa kisheria, lakini Takukuru wanajadili
mpaka kesi za jinai.
Alisema kujadili ripoti ya Takukuru, kungewezesha kuweka wazi watuhumiwa kwa asilimia 70, wakati ile ya CAG ni asilimia 30 tu.
Kafulila
alisema baada ya kuzuiwa kutoa hoja yake binafsi, anajadiliana na
wanasheria wake kuangalia taratibu za kikanuni ndani ya mamlaka ya
Bunge, ili kupata ushauri nini cha kufanya.
Suala
hilo la utoaji wa fedha takribani Sh bilioni 200, kwa iliyokuwa akaunti
ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT), baada ya kuamuliwa,
Serikali, Bunge na Mahakama vilipewa maazimio ya kutekeleza.
Tayari
kwa upande wa Serikali, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka aliondolewa katika nafasi yake, huku
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema na aliyekuwa Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, wakijiuzulu.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment