
SERIKALI imesema itaendelea kuboresha sekta ya afya nchini kwa kuboresha zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, rufaa na vyuo vinavyotoa taaluma ya uuguzi na udaktari.
Itafanya hivyo ili kuwezesha asilimia kubwa ya wagonjwa kutibiwa hapa nchini badala ya kwenda nje ya nchi.
Rais Jakaya Kikwete amesema hayo wakati akifungua jengo la upasuaji katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi na kuweka jiwe la msingi la wadi ya wanawake na watoto katika hospitali hiyo.
Alisema kwa kipindi cha takribani miaka 10, sekta ya afya nchi imeendelea kuimarika na kuwezesha kupatikana kwa wataalamu wa sekta ya afya, hatua ambayo imeendelea kusaidia kutatua matatizo ya afya kwa Watanzania.
Alisema katika kufanikisha suala la upasuaji wa moyo, serikali ilipeleka wataalamu kwenda kujifunza zaidi nchini India huku baadhi ya wataalamu wa nje wakisaidia wataalamu wa hao nchini kufanikisha upasuaji huo.
Rais alisema mpango mwingine ni kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambacho kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 5,000 wa fani mbalimbali za tiba, ambapo mwaka jana walihitimu na idadi kama hiyo inatarajiwa kuzalishwa mwaka huu.
Kwa upande wa Muhimbili, miaka iliyopita walikuwa 250 na sasa ni takribani 300. Ujenzi wa chuo eneo la Mloganzila na hospitali unaendelea, baada ya wakazi wa eneo hilo kulipwa fidia.
Hospitali hiyo ya Mloganzila itakuwa na vitanda 600 na Chuo cha Mloganzila kitakachokuwa tawi la Chuo Kikuu cha Muhimbili, kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi zaidi ya 12,000 wa fani mbalimbali.
“Wastani wa daktari mmoja kwa upande wa Tanzania ni wagonjwa 30,000 na muuguzi mmoja ni wagonjwa 23,000, ingawa takwimu za kimataifa zinataka daktari mmoja kwa wagonjwa 500, hivyo hivyo kwa wauguzi,” alisema.
Kwa upande wake naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Stephen Kebwe alisema mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa matumizi ya uzazi wa mpango.
Alisema mkoa umefikia asilimia 67 ya chanjo, ikiwamo ya shingo ya kizazi na asilimia 90 ya wajawazito wanajifungua kupitia wataalamu wa afya.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment