Watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wanaoishi vijijini, wana hatari ya kupata magonjwa ya saratani ya ngozi, kutokana na kutokuwa na elimu ya afya bora na utunzaji wa ngozi.
Kauli
hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu wa Ngozi mkoani
Dodoma, Ludovick Kowo, katika warsha ya mafunzo ya afya bora na utunzaji
wa ngozi kwa albino wilayani Kongwa.
Alisema
kutokana na ukosefu wa elimu ya utunzaji wa afya ya ngozi kwa walemavu
waishio vijijini, walemavu hao wana hatari kubwa ya kupatwa na saratani
ya ngozi na kuongeza kuwa ukosefu huo wa elimu, unatokana na umasikini.
Pia
alisema walemavu walio wengi, hawana elimu ya kutosha ya utunzaji wa
afya zao, hali inayochangiwa na ukosefu wa kipato cha kuwasaidia katika
kujikwamua na hali ngumu na ununuzi wa dawa hizo.
Akizungumza
kwenye mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la
Kufadhili Asasi za Kiraia (FCS), Kowo alisema Sh milioni 45 zimetolewa
kwa ajili ya utoaji wa elimu ya afya bora na utunzaji wa ngozi.
Alisema
ufadhili huo utaziwezesha wilaya mbili ikiwemo ya Kongwa na Mpwapwa na
kata 12 kupata elimu itakayowasaidia kuepukana na magonjwa hayo, ambayo
yamekuwa tishio na kusababisha vifo.
Mwenyekiti huyo amezitaka taasisi na mashirika na serikali,
kuwezesha walemavu kwa kuwapa mitaji, itakayowawezesha kuunda vikundi vya ujasiriamali ili waondokane na hali ngumu ya maisha.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment