Mikoa sita 'imevurunda' katika ujenzi wa maabara katika shule za sekondari baada ya kushindwa kufikia malengo. Ni mikoa mitatu pekee ndiyo imefanya vizuri kwa kuvuka nusu ya malengo.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda alitaja mikoa ambayo haikufika hata robo ya malengo
kuwa ni Mtwara (asilimia 21), Lindi (asilimia 20), Tabora (asilimia
17), Dodoma (asilimia 12), Rukwa (asilimia 11) na Kigoma (asilimia 10).
“Tunaweza
kusema hii ndiyo mikoa ya mwisho katika kutekeleza agizo la Rais.
Mikoa 16 ambayo sikuitaja hapa iko katika kundi la asilimia kati ya 26
hadi 49,” alisema Pinda kupitia hotuba yake ya kuahirisha Bunge la 18.
Pinda
alitaja mikoa mitatu iliyofanya vizuri kuwa ni Njombe uliofanikiwa
kukamilisha ujenzi kwa asilimia 96 wa maabara za shule za sekondari,
Ruvuma iliyokamilisha kwa asilimia 81 na Morogoro ambao ni watatu kwa
kujenga vyumba kwa asilimia 53.
Waziri Mkuu alipongeza Ruvuma na Njombe kwa kutekeleza vizuri maelekezo ya Rais, akisema imeonesha mfano mzuri.
Alisema Morogoro ni wa tatu. Alisema Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi, Desemba 31 mwaka jana, aliongeza miezi sita zaidi hadi Juni 2015 kwa ambao hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo, ili wakamilishe.
Alisema Morogoro ni wa tatu. Alisema Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa wananchi, Desemba 31 mwaka jana, aliongeza miezi sita zaidi hadi Juni 2015 kwa ambao hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo, ili wakamilishe.
Pinda
alisema matarajio ya Rais Kikwete ni kwamba muda huo unatosha kwa kila
sekondari nchini kuwa na vyumba vitatu vya maabara .
“Hivyo,
ninawataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, mameya, wenyeviti na
wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya na miji nchini
kuhakikisha maagizo haya yanatekelezwa. Aidha, ninatoa rai kwa
waheshimiwa wabunge na madiwani kutoa msukumo stahiki katika utekelezaji
wa maagizo haya kwa maslahi ya Taifa letu,” alisema.
Kwa
upande wa Serikali, Pinda alisema Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi), haina budi kuhakikisha agizo
linatekelezwa ndani ya muda uliotolewa; yaani Juni mwaka huu.
Aidha,
alisisitiza katika usimamizi, Tamisemi ihakikishe vyumba vya maabara
vinavyojengwa vinakuwa na ubora stahiki na vinalingana na thamani ya
fedha zilizotumika.
Amesema ubadhirifu wa aina yoyote usipewe nafasi na watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua za kisheria mapema.
“Nitapenda Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi waendelee kufuatilia suala hili na kunipa taarifa mara kwa mara,” alisema.
Mwaka
2012, Rais Kikwete akiwa ziarani katika mkoa wa Singida, alielekeza
kila shule ya sekondari nchini iwe ina vyumba vitatu vya maabara ifikapo
Novemba 30, 2014.
Tangu
wakati huo hadi sasa, utekelezaji unaendelea na kwa mujibu wa Waziri
Mkuu, hali ya ujenzi wa vyumba vya maabara inaonesha hadi Desemba
mwaka jana, vyumba 3,607 sawa na asilimia 34 ya mahitaji ya vyumba
10,653 vya maabara nchini vilikuwa vimejengwa.
Aidha,
vyumba 6,249 sawa na asilimia 59 ya mahitaji, vilikuwa vinaendelea
kujengwa na asilimia saba vilikuwa havijaanza kujengwa.
Wakati
huo huo Pinda alisema bajeti ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la
Wapigakura ni Sh bilioni 218 na ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, ni Sh
bilioni 268.
“Naelewa
kwamba changamoto kubwa ni upatikanaji wa fedha hizi kwa muda muafaka.
Hata hivyo, kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha kwamba fedha
zinapatikana na kazi hii muhimu inafanyika kama ilivyopangwa,” alisema.
Kuhusu
Katiba Inayopendekezwa, Waziri Mkuu alitoa mwito kwa wakuu wa mikoa
wote nchini, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu usambazaji wa nakala
zake.
Aidha
ametaka wananchi wahimizwe kusoma Katiba hiyo, ili washiriki kikamilifu
katika upigaji kura ya maoni utakaofanyika Aprili 30 mwaka huu.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment