Mtoto Yohana Bahati mwenye ulemavu wa ngozi (albino), aliyetekwa katika Kijiji cha Ilelema wilayani Chato katika Mkoa wa Geita, mwili wake umekutwa ukiwa umefukiwa huku umenyofolewa miguu na mikono.
Polisi
imesema baba mzazi wa mtoto huyo, Bahati Misalaba na mkazi wa kitongoji
cha Mapinduzi katika kijiji cha Lumasa, wilayani Chato, wamekamatwa kwa
ajili ya uchunguzi zaidi.
Mwili
wa mtoto huyo mwenye umri wa mwaka na miezi sita, ulikuwa umefukiwa
katika moja ya mashamba ya mahindi ndani ya hifadhi, huku pembeni yake
kukiwa na kipande cha nguo kilichokuwa kimejaa damu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba mwili ulipatikana juzi saa 12 jioni.
''Mwili
wa mtoto huyu ulipatikana ukiwa umefukiwa ndani ya kaburi dogo katika
shamba la mahindi, mahali ambapo si makazi rasmi ya kuishi watu wakati
jeshi la polisi kwa kushirikiana na raia wema walipokuwa katika harakati
za kumtafuta baada ya kuwa ameibwa siku ya Jumapili saa 2.00 usiku
akiwa amebebwa na mama yake,'' alisema Kamanda Konyo.
''Eneo
jirani na lilipokuwa kaburi la mwili wa mtoto huyu kulikutwa kipande
cha nguo chenye damu, lakini polisi walipofukua walikuta miguu yote na
mikono ikiwa imenyofolewa, hali iliyotulazimu kuamini kuwa watekaji
waliofanya ukatili huo watakuwa wameondoka na viungo hivyo,'' alisema.
Katika
tukio hilo, watekaji waliokuwa na silaha mbalimbali za jadi,
walimjeruhi pia Ester Bahati (30), ambaye ni mama wa mtoto. Kwa sasa
Ester amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
''Msako
tuliouendesha ulilenga kuokoa maisha ya mtoto huyu, lakini hatukuweza
kufanikiwa katika hilo badala yake tumempata akiwa tayari
amekwishafariki, hili ni tukio baya sana, lenye kuudhi lililojaa ukatili
usioweza kuvumilika kwa mtu yeyote anayeamini katika Mungu,” alisema kamanda.
Aliahidi, “Tutaendelea
kuwasaka wale wote waliohusika katika tukio hili, wakiwemo waganga wa
jadi, naamini tutawakamata na siyo muda mrefu hakuna atakayebaki salama
katika hili.''
Alitoa
mwito kwa wananchi kutoruhusu tukio lingine la namna hiyo litokee,
badala yake wachukue hatua mapema kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika
vya dola viweze kudhibitiwa.
Alisema kila mtu anapaswa kutambua wajibu kuwa ulinzi na usalama ni suala la jamii nzima na siyo kuachia polisi peke yake.
Aidha alitaka waandishi wa habari kusaidia kuibua matishio mbalimbali wanapokuwa wanatimiza majukumu yao hatua zichukuliwe.
Kwa
mujibu wa taarifa kutoka kijijini, familia anayotoka mtoto huyo ina
watoto wengine wawili wenye ulemavu wa ngozi ambao ni Tabu Bahati (3) na
Shida Bahati (12).
Wakati
wa utekaji, watoto hao inaelezwa hawakuwa nyumbani hapo, bali walikuwa
wakicheza nyumba ya jirani. Baba yao inadaiwa alikuwa nyumbani akiota
moto.
Mama yao, Ester anaendelea kutibiwa majeraha yaliyotokana na mapanga wakati akijaribu kumwokoa mtoto wake.
Hii
ni mara ya pili ndani ya kipindi kisichozidi miezi miwili, tangu tukio
kama hilo lijitokeze baada ya mtoto Pendo wa kijiji cha Ndami, Wilaya ya
Kwimba, mkoani Mwanza, kutekwa na watu wasiofahamika. Mtoto huyo hadi
sasa hajapatikana.
Mratibu
wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini na Mkurugenzi Mkazi wa
Shirika la Maendeleo la umoja huo (UNDP), Alvaro Rodriguez amehimiza
serikali kuchukua hatua zaidi, kukabili mauaji ya watu wenye albinism.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuhusu kuuawa kwa mtoto Yohana,
Mratibu huyo wa UN alisema pamoja na juhudi zilizopo sasa za kukabili
mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu huo wa ngozi, lazima ziongezwe.
Alisema
katika kipindi cha miezi miwili, Tanzania imeshuhudia kutekwa nyara kwa
watoto wawili katika Kanda ya Ziwa, akiwemo Pendo ambaye pamoja na
juhudi za kumtafuta kuendelea, hadi sasa hajajulikani aliko.
Alisema Umoja wa Mataifa unasikitishwa na vitendo vya kikatili dhidi ya watoto hao wawili.
Mashambulio
dhidi ya watu wenye albinism, yanaelezwa kuwa yanasababishwa na imani
za kishirikina na kwamba kutoka mwaka 2000 hadi sasa, watu 74 wenye
ulemavu huo wameuawa.
“Mashambulizi
haya yanaambatana na ukatili mkubwa, na wakati serikali inafanya kila
juhudi kukabili tatizo hili, juhudi kubwa zinastahili kufanywa ili
kukomesha mauaji na kulinda kundi hilo dogo la watu ambao wako katika
hatari kubwa," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema mashambulio dhidi ya albino, hayavumiliki, si halali kwa namna yoyote na yanaweza kukomeshwa.
Mratibu huyo alipongeza juhudi za serikali katika kukabiliana na wimbi hilo la mauaji hayo.
Alisema Umoja wa Mataifa unataka mamlaka husika, kuhakikisha haki za raia zinalindwa na utawala wa sheria unazingatiwa.
“Tunataka mwaka 2015 kuwa mwaka wa haki za Watanzania wote zitaheshimiwa wakiwemo albino,” ilisisitiza.
Mratibu
huyo wa UN alisema amezungumza na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Fatma Mwassa
na Chama cha Maalbino ( TAS). Alisema alihakikishiwa kwamba wanafanya
kila linalowezekana, kukomesha madhila dhidi ya maalbino.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment