Tukio la takribani wiki mbili zilizopita
lililofanywa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven
Wassira, (pichani) la kukosea kufunga vifungo vya koti lake katika
mkutano wa Injili wa dhehebu la Wasabato uliofanyika Februari 7, mwaka
huu, limeipa lawama kambi ya kusaka urais inayoongozwa na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernand Membe.
Wafuasi wa Waziri Wassira, ambaye kama Membe, naye ametangaza nia
yake ya kuwania kuteuliwa na CCM ili kupeperusha bendera yake katika
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, wanaamini maofisa wa Wizara ya Membe,
waliisambaza picha hiyo makusudi, kwani walikuwa na picha zingine
zilizopigwa baada ya kuwa amerekebisha uvaaji wake.
“Ni kweli kipindi cha mwanzo sikuweka vizuri vifungo vya koti langu,
ila baada ya kuambiwa hilo na mzee Kuboja nililiweka sawa, sasa
nashangaa ofisi ya huyo jamaa yangu inasambaza picha ya awali ili tu
kunidhalilisha. Kwa kweli nimehuzunika sana, nimefadhaika sana, na
nimejua kwamba hizi mbio za urais wengine wanazitumia kama nafasi ya
kuwachafua wenzao,” alinukuliwa Wassira akisema, mara tu baada ya picha
hizo kuanza kuonekana katika mitandao ya kijamii.
Wafuasi wake ambao
wanaamini kuvuja kwa picha hiyo kumemharibia katika harakati zake, walisema
kambi ya Membe ina hofu na nguvu za mtu wao, ndiyo maana wametumia fursa
hiyo kumdhalilisha.
“Hapa hatumlaumu Waziri Membe, inawezekana kabisa yeye hahusiki na
hajui lolote, ila kwa vyovyote hawa ni wapambe wake ambao huenda
wanamuona Wassira kama tishio kwa mtu wao, wanaamua kufanya hivi
wakiamini itasaidia kumshusha, hamna kitu,” alisema mpambe mmoja
aliyekataa kutaja jina lake, kwa kile alichodai kulinda masilahi yake.
Wakati muda wa kuanza kwa hatua za uteuzi ukiwa unakaribia, vita
kubwa inaendelea ndani ya CCM baina ya watu mbalimbali waliotangaza nia
ya kuwania nafasi hiyo kwa lengo la kumrithi Rais Jakaya Kikwete
anayemaliza kipindi chake cha miaka kumi mwaka huu. Vita hivyo
vinaambatana na kuchafuana kwa namna mbalimbali, ikiwemo uzushi, kejeli
na kashfa.
Tukio la Waziri Wassira lilitokea siku hiyo wakati wa zoezi la kupiga
picha ya pamoja na kiongozi wa dhehebu la Wasabato duniani ambaye
alikuwa nchini katika ziara rasmi.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment