Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameeleza sababu za Bunge kushindwa kujadili miswada kadhaa, ikiwemo uliohusu Marekebisho ya Sheria ya Kiislamu, inayotambua Mahakama ya Kadhi.
Akihitimisha
shughuli za mkutano wa 18 wa Bunge jana, Pinda alisema muswada huo
umesogezwa mbele, ili Kamati ya Bunge ipate nafasi na muda wa kupitia na
kutoa ushauri kwa Bunge.
Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 2 wa mwaka 2014,
unaohusu Muswada wa Marekebisho ya Sheria hiyo ya Kiislamu Sura 375 ni
miongoni mwa ambayo haikujadiliwa.
Mingine
iliyopangwa kujadiliwa katika mkutano huo wa Bunge, ni Muswada wa
Sheria ya Usimamizi wa Kodi wa mwaka 2014 na Muswada wa Sheria ya
Takwimu wa mwaka 2013.
“Hatukuweza
kuijadili miswada hiyo katika mkutano huu, ili Kamati husika zipate
nafasi na muda wa kupitia na kutoa ushauri kwa Bunge lako Tukufu.
“Ni
matumaini yangu kwamba miswada hii itapata nafasi ya kuwasilishwa na
kujadiliwa katika mkutano ujao wa 19 wa Bunge lako Tukufu,” alisema Pinda.
Katika
mkutano huo, wabunge walipokea na kujadili taarifa mbalimbali
zilizowasilishwa na Kamati za Bunge za kisekta na zisizo za kisekta.
Wakati
huo huo katika hotuba yake, Pinda aliwaambia wabunge kwamba hali ya
uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini kwa ujumla, imeendelea kuwa
ya kuridhisha katika maeneo mengi, kutokana na mavuno mazuri katika
msimu wa kilimo wa 2013/2014.
Kuhusu
mwenendo wa malipo ya madeni ya ununuzi wa mahindi kwa msimu wa
2014/2015, Pinda alisema hadi kufikia Desemba 2014 Serikali ilikuwa
inadaiwa Sh bilioni 89 na wakulima waliouuzia Wakala wa Taifa wa Hifadhi
ya Chakula (NFRA) mahindi.
Hadi
kufikia Januari 29 mwaka huu, kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali
ilikuwa imelipa wakulima hao Sh bilioni 15 na kubakiza deni la Sh
bilioni 74.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment