MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra)
imeshikwa kigugumizi kuhusu suala la kushusha nauli ya magari ya abiria
kwa kutoa sababu za kisheria pamoja na ukokotoaji wa tozo.
Ikasema, kwa mujibu wa Kanuni za Tozo pamoja na Sheria, Sumatra
inapaswa kurejea tozo ya huduma baada ya mtoa huduma au mtumiaji wa
huduma kupitia Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa
na Sumatra (Sumatra CCC) kuwasilisha maombi.
Pia huridhia viwango kwa kuzingatia masuala yote yanayoathiri gharama
za uendeshaji, mafuta ikiwa ni moja ya eneo muhimu katika kukokotoa
tozo zinazostahili kuridhiwa.
Meneja Mawasiliano kwa Umma, David Mziray alisema mwasilishaji wa
maombi awe ni mtoa huduma au Sumatra CCC anapaswa atoe maelezo ya kina
kuhusu sababu za kuomba mabadiliko ya tozo, jinsi alivyoathirika, ikiwa
ni pamoja na kuambatisha nyaraka muhimu zinazoweza kuthibitisha hoja
zake.
Alisema maoni ya wadau huzingatiwa kwa pamoja na masuala
yaliyoainishwa katika Sheria ya Sumatra ambayo inatoa muongozo wa
masuala ya kuzingatia katika kuridhia viwango vya tozo mbalimbali.
Alisema masuala hayo ni pamoja na gharama za uendeshaji, haja ya
kukuza ushindani katika soko na kulinda maslahi ya watumia huduma na
watoa huduma.
Akizungumzia kuridhia viwango kwa kuzingatia masuala yote
yanayoathiri gharama za uendeshaji wanazingatia umuhimu wa kuwa na
huduma endelevu, kulinda maslahi ya watumiaji na watoa huduma kwa kuweka
mizania sawa na gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na mishahara na
gharama za matengenezo.
Pia gharama za vipuri na matairi, gharama zaununuzi wa mabasi, riba
kutokana na mikopo, gharama za bima, mafuta navilainishi, gharama
nyingine za kiutawala, kodi na tozo mbalimbali, athari za viashiria vya
kiuchumi kama mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya shilingi na
kujenga mazingira ya ushindani.
Mziray alisema lengo la Sumatra katika kupanga nauli ni kuona pamoja
na mambo mengine kuwa katika viwango vinavyoridhiwa kuna kuwa na
ushindani zaidi miongoni mwa watoa huduma na hivyo kuwa na huduma bora
zaidi na endelevu.
“Ni vyema kutambua kuwa kwa kiasi kikubwa huduma za usafiri wa umma
zinatolewa na sekta binafsi, wengi wao wenye kipato cha kawaida. Hivyo
basi nauli inayolipwa na abiria ndiyo inayolipia gharama za uendeshaji
na kumpa mtoa huduma uwezo ili huduma iwe endelevu na kuvutia wawekezaji
zaidi kuingia katika biashara hiyo,” alisema.
Alisema katika mazingira ambayo watoa huduma wamekuwa wakijielekeza
katika kupata faida iliyokithiri, Sumatra imekuwa na jukumu la
kuhakikisha kuwa mtumia huduma analindwa dhidi ya nauli kubwa kupita
kiasi ambayo inaweza kumfanya mtumiaji huduma kushindwa kutumia huduma
hiyo.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment