Muswada wa Sheria ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara hautajadiliwa katika mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma baada ya serikali kuuondoa kwa maandalizi zaidi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema jana usiku kuwa wameamua kuuondoa muswada huo ili kupata fursa ya kutoa elimu zaidi kwa viongozi wa dini na kuufanyia marekebisho baadhi ya maeneo.
Alisema
serikali inatarajia kuurejesha tena bungeni mwezi ujao. Hata hivyo,
habari za uhakika kutoka Dodoma zinasema kuwa kulikuwa na mvutano mkali
ndani ya kamati ya Bunge iliyokuwa inashughulikia muswada huo uliokuwa
kwa misingi ya imani hivyo busara ilitumika kuahirishwa uwasilishwaji
kwa mara ya pili kwani mjadala kwenye Bunge zima ungeweza kuleta
mpasuko.
Muswada
huo ulikuwa unawasilishwa kutokana na ahadi ya serikali kwenye Bunge
Maalum la Katiba ambako mjadala ulikuwa mzito baadhi ya wajumbe wakitaka
mahakama ya kadhi iingizwe kwenye Katiba Inayopendekezwa, lakini Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, akashauri kutungwa kwa sheria ya mahakama hiyo,
badala ya kuuingiza kwenye katiba.
Tangu
serikali itangaze kuwa itawasilisha muswada huo bungeni, kumekuwa na
mvutano ndani ya jamii, kundi moja likiupinga kwa madai kuwa serikali
haipaswi kujihusisha na masuala ya dini kama katiba inavyoelekeza.
Ilielezwa kwamba kama Waislamu wanahitaji mahakama hiyo, basi waunde kwa
njia zao wenyewe bila kuhusisha serikali.
Hata
hivyo, serikali ilisema kuwa imeandaa muswada huo ili kuweka utaratibu
wa kuundwa kwa mahakama hizo kisheria, lakini suala la uendeshaji wake
na gharama hazitabebwa na serikali bali Waislamu wenyewe.
Tayari
jumuiya za Kikristo kupitia maaskofu wao wamekwisha kutoa msimamo wao
juu ya mahakama hizo wakisema kuwa siyo jukumu la serikali kuzianzisha.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment