Marais watano wa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Jakaya Kikwete wa Tanzania na mwenyeji wa mkutano Uhuru Kenyatta wa Kenya.





*** Rais Jakaya Kikwete amekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akichukua jukumu hilo kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta aliyemaliza muda wake.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika mkutano wa 16 wa wakuu hao wa nchi hizo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Jomo Kenyatta.
Jana,
nchi hizo zilizindua mfumo wa mawasiliano ya pamoja ambapo Rais Kikwete
aliwasiliana na Balozi Sefue na kuzungumza naye mambo machache.
Marais wengine wa nchi hizo wanachama pia walifanya hivyo kwa kuwasiliana na mataifa yao.
Wizara
ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilizindua mfumo huo ambao
utaziwezesha nchi wanachama kupunguza gharama za uendeshaji wa mikutano
baina ya wajumbe wao.
Awali, wajumbe walilazimika kusafiri na kukutana sehemu moja.
Awali, wajumbe walilazimika kusafiri na kukutana sehemu moja.
Akielezea mfumo huo, Mkurugenzi Msaidizi
wa Huduma za Jamii wa wizara hiyo, Eliabi Chodota alisema kuwa,
utasaidia kupunguza gharama katika mikutano mbalimbali inayofanyika
baina ya wajumbe wa nchi wanachama.
“Mfumo huu utaondoa
haja ya wajumbe kukutana. Marais, mawaziri, makatibu wakuu pamoja na
wafanyakazi wa Serikali wataendesha mikutano yao bila ya kukutana. Hii
itapunguza matumizi ya fedha kwa ajili ya kujikimu na bajeti nyingine za
mikutano,” alisema Chodota.
Alifafanua kuwa wanyakazi
wa taasisi mbalimbali zinazoshirikiana wataweza kutatua matatizo
yatakayojitokeza kwa kutumia mfumo huo jambo litakaloongeza ufanisi
katika utatuzi wa kero ndogo ndogo zinazowakumba wananchi wa mataifa
wanachama.
Awali, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue alisema hafahamu sababu ya Kenya kuzuia magari yenye usajili wa
Tanzania kufika na kuingia Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta
nchini humo.
Balozi Sefue alisema hayo alipozungumza
na gazeti hili katika ofisi za Wizara ya Afrika Mashariki (EAC),
alikohudhuria uzinduzi wa mfumo wa kuendesha mikutano kwa njia ya video
(video conferencing) uliokuwa ukifanyika Kenya.
Alisema
Serikali inashangaa kuona zuio hilo linafanyika wakati mkataba wa
ushirikiano katika sekta ya utalii baina ya nchi hizi mbili ulisainiwa
mwaka 1985 na kubainisha vipengele vitakavyohusika.
“Mazungumzo
yanaendelea ili kurekebisha tatizo lililojitokeza. Tumeshtushwa na zuio
hilo licha ya kuwapo kwa mkataba unaoruhusu jambo hilo. Mpaka sasa
hawajatuambia tatizo ni nini lililowafanya wazuie magari yetu,” alisema.
Katika
hatua nyingine, suala la mgogoro huo wa kibiashara uliosababisha Kenya
kuzuia magari maalumu ya watalii na abiria yenye namba za usajili za
Tanzania kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA)
kushusha na kupakia abiria limefikishwa kwenye baraza la mawaziri wa
kisekta wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwenye kikao kilichofanyika
juzi jijini hapa.
Katika kikao hicho kilichoongozwa na
mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe kilijadili mambo mbalimbali ya kisekta
na mawaziri kutoka nchi za Rwanda, Burundi, Kenya, Tanzania na Uganda na
nchi hizo mbili kuamua suala hilo linafaa kujadiliwa baina yao pekee
yao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utali, Dk
Adelhim Meru alithibitisha kikao hicho kufanyika na kusema hakikujadili
mgogoro huo baada ya kukubaliana ujadiliwe baina ya nchi za Kenya na
Tanzania katika mkutano utakaofanyika jijini Arusha, Machi 18 hadi 20
mwaka huu.
“Serikali zetu mbili zimeona ni busara
tukawa na vikao vyetu wenyewe ambavyo kimsingi vilishaanza badala ya
kuwashirikisha wanachama wengine wa EAC, ambao jambo hili haliwahusu
moja kwa moja,” alisema Dk Meru.
Mgogoro huo ulianza
Desemba mwaka jana baada ya Kenya kuyazuia magari ya Tanzania kufika
moja kwa moja JKIA kupeleka abiria na kuwachukua kwa madai kuwa nchi
hizo zina makubaliano ya mwaka 1985, inayozuia magari ya kitalii
kutoingia kwenye vivutio vya kitalii vya nchi husika jambo ambalo Waziri
wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alilipinga kuwa viwanja vya
ndege siyo sehemu za kitalii kwa mujibu wa makubaliano hayo.
Mmoja
wa wafanyabiashara wa muda mrefu wa magari yanayofanya safari zake
katika miji ya Nairobi na Arusha, James King’ori alisema utaratibu
uliowekwa na Serikali ya Kenya umekuwa ukiwagharimu fedha zaidi kwani
wanapofika sehemu waliyopangiwa hulazimika kukodi magari mengine ya
kuwafikisha wageni wao uwanja wa ndege na kuwachukua waliowasili kwa
utaratibu huo.
Waziri Nyalandu alisema inakadiriwa
abiria 300,000 hutumia Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini
Nairobi kuingia na kuondoka Tanzania kutokana na ubora wa miundombinu
yake na wepesi wa kuunganisha safari katika nchi mbalimbali ulimwenguni.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment