Waafrika wanaoishi na kusoma jijini hapa, wameshiriki na wenyeji katika sherehe za mwaka mpya wa China (Spring Festival) unaoadhimishwa kwa wiki moja kuanzia Februari 19 mwaka huu.
Walisherehekea
mwishoni mwa wiki badala ya wakati husika kutokana na juma hilo kuwa na
shughuli nyingi za China na pia watu wengi wakiwemo wenyeji husafiri
nje ya miji kama Beijing kwa likizo muhimu ambayo wengi huipata mara
moja kwa mwaka.
Sherehe
hizo za Waafrika zilifanyika katika Kituo cha Kiafrika cha Beijing
(BeijingAfrican Center) mjini hapa na kuhudhuriwa na watu mbalimbali
kutoka mataifa ya Afrika na wenyeji Wachina.
Mratibu
wa sherehe hizo na mwasisi wa kituo hicho, Tracy Qi ambaye ameishi
Afrika Kusini kwa miaka 15, alisema lengo la sherehe hizo ni kuunganisha
China na nchi za Afrika katika masuala muhimu ya kiutamaduni, kiuchumi
na kijamii.
“Tunatengwa
na mipaka ya kijiografia lakini sisi sote ni ndugu, nimeishi Afrika
Kusini nusu ya maisha yangu nilionayo kwa sasa, nimefika Tanzania pia,
hivyo ninawafahamu Waafrika walivyo wakarimu na wenye upendo, nia ya
sherehe hizi ni kuwaleta watu pamoja, kufurahia na kujifunza tofauti
zetu ili tuishi salama na kwa upendo,” alisema Qi.
Katika
sherehe hizo, vyakula mbalimbali vya Kiafrika ikiwamo ugali, maharage,
samaki, kisamvu, nyama za utumbo, sambusa, chapati na pilau pamoja na
kahawa vilipikwa na wanafunzi wa Kiafrika kutoka Tanzania, Kenya,
Msumbiji na Zimbabwe na kusababisha watu kugombea wakitaka kuhakikisha
wanakula kila aina ya chakula cha Kiafrika. Kahawa iliandaliwa na
wananchi wa Ethiopia.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mawasiliano cha China (CUC) na Mkurugenzi wa Kituo
cha Utafiti cha Afrika chuoni hapo, Profesa Zhang Yangiu aliyewaongoza
wanafunzi wa Kiafrika kupika na kushiriki sherehe hizo, alisema ni fursa
nzuri kujifunza utamaduni wa Kiafrika kwa kuwa nchi nyingi za Afrika ni
rafiki wa kindugu wa China.
Nao
wanafunzi wa CUC walioshiriki sherehe hizo, walisema kwa nyakati
tofauti kuwa, wamejifunza mambo mengi na wakapendekeza kila mara kuwepo
na hafla ya kuwakutanisha na wenyeji (Wachina) ili kueleza zaidi mazuri
ya Afrika na kutoa nafasi ya wananchi wa China kulielewa Bara la Afrika
zaidi.
“Fursa
hii ni ya pekee, inapaswa kuendelezwa, tukutanishwe kwa mijadala,
tuelezane masuala yanayotuhusu, tuifahamu China na Wachina wazifahamu
nchi zetu maana wengi wanadhani Afrika ni nchi moja kumbe hawajui ni
zaidi ya nchi 52,” alisema James Mwita kutoka Kenya.
Facebook Blogger Plugin by AllyTz
Post a Comment